John 7

Kutokuamini Kwa Ndugu Zake Yesu

1 aBaada ya mambo haya, Yesu alikwenda sehemu mbalimbali za Galilaya. Hakutaka kwenda Uyahudi kwa sababu Wayahudi huko walitaka kumuua. 2 bSikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. 3 cHivyo ndugu zake Yesu wakamwambia, “Ondoka hapa uende Uyahudi ili wanafunzi Wako wapate kuona miujiza unayofanya. 4Mtu anayetaka kujulikana hafanyi mambo yake kwa siri. Kama unafanya mambo haya, jionyeshe kwa ulimwengu.” 5 dHata ndugu zake mwenyewe hawakumwamini.

6 eYesu akawaambia, “Wakati wangu bado haujawadia, lakini wakati wenu upo siku zote. 7 fUlimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini unanichukia mimi kwa sababu ninawashuhudia kwamba matendo yao ni maovu. 8 gNinyi nendeni kwenye Sikukuu, lakini mimi sitahudhuria Sikukuu hii kwa sababu wakati wangu haujawadia.” 9Akiisha kusema hayo, akabaki Galilaya.

Yesu Kwenye Sikukuu Ya Vibanda

10Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alikwenda lakini kwa siri. 11 hWayahudi walikuwa wakimtafuta huko kwenye Sikukuu na kuulizana, “Yuko wapi huyu mtu?”

12 iKulikuwa na minongʼono iliyoenea kumhusu Yesu katika umati wa watu, wakati wengine wakisema, “Ni mtu mwema.”

Wengine walikuwa wakisema, “La, yeye anawadanganya watu.”
13 jLakini hakuna mtu yeyote aliyemsema waziwazi kumhusu kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi.

Yesu Afundisha Kwenye Sikukuu

14 kIlipokaribia katikati ya Sikukuu, Yesu alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha. 15 lWayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?”

16 mNdipo Yesu akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma. 17 nMtu yeyote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe. 18 oWale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake. 19 pJe, Mose hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”

20 qUle umati wa watu ukamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?”

21 rYesu akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu. 22 sLakini kwa kuwa Mose aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Mose bali kwa baba zenu wakuu), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato. 23 tIkiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi sheria ya Mose isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato? 24 uAcheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”

Je, Yesu Ndiye Kristo?

25 vNdipo baadhi ya watu wa Yerusalemu wakawa wanasema, “Tazameni, huyu si yule mtu wanayetaka kumuua? 26 wMbona yuko hapa anazungumza hadharani na wala hawamwambii neno lolote? Je, inawezekana viongozi wanafahamu kuwa huyu ndiye Kristo?
Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.
27 yTunafahamu huyu mtu anakotoka, lakini Kristo atakapokuja, hakuna yeyote atakayejua atokako.”

28 zNdipo Yesu, akaendelea kufundisha Hekaluni, akisema, “Ninyi mnanifahamu na kujua nitokako. Mimi sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni wa kweli na ninyi hammjui. 29 aaMimi namjua kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye alinituma.”

30 abNdipo wakatafuta kumkamata, lakini hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijawadia. 31 acNao watu wengi wakamwamini, wakasema, “Je, Kristo atakapokuja, atafanya miujiza mikuu zaidi kuliko aliyoifanya mtu huyu?”

Walinzi Wanatumwa Kumkamata Yesu

32Mafarisayo wakasikia watu wakinongʼona mambo kama hayo kuhusu Yesu, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata.

33 adYesu akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma. 34 aeMtanitafuta lakini hamtaniona, nami niliko ninyi hamwezi kuja.”

35 afWayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani? 36 agYeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona,’ na, ‘nami niliko ninyi hamwezi kuja’?”

Mito Ya Maji Ya Uzima

37 ahSiku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe. 38 aiYeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.” 39 ajYesu aliposema haya alimaanisha Roho Mtakatifu ambaye wote waliomwamini wangempokea, kwani mpaka wakati huo, Roho alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Yesu alikuwa bado hajatukuzwa.

Mgawanyiko Miongoni Mwa Watu

40 akWaliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa ule umati wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.”

41 alWengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!”

Lakini wengine wakauliza, “Je, Kristo kwao ni Galilaya?
42 amJe, Maandiko hayasemi kwamba Kristo atakuja kutoka jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?” 43 anKwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Yesu. 44 aoBaadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa.

Kutokuamini Kwa Viongozi Wa Wayahudi

45 apHatimaye wale walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliokuwa wamewatuma ili kumkamata Yesu, wakaulizwa, “Mbona hamkumkamata?”

46 aqWale walinzi wakajibu, “Kamwe hajanena mtu yeyote kama yeye anenavyo.”

47 arMafarisayo wakajibu, “Je, nanyi pia mmedanganyika? 48 asJe, kuna kiongozi yeyote au mmoja wa Mafarisayo ambaye amemwamini? 49Lakini huu umati wa watu wasiojua Sheria ya Mose, wamelaaniwa.”

50 atNdipo Nikodemo, yule aliyekuwa amemwendea Yesu siku moja usiku, ambaye alikuwa mmoja wao akauliza, 51 au“Je, sheria zetu zinaturuhusu kumhukumu mtu kabla ya kumsikiliza na kufahamu alilotenda?”

52 avWakamjibu, “Je, wewe pia unatoka Galilaya? Chunguza nawe utaona kwamba hakuna nabii atokae Galilaya!” [ 53Kisha wakaondoka, kila mtu akarudi nyumbani kwake.

Copyright information for SwhNEN